‘Kwenye sekta ya korosho kuna fursa ya kipato, ajira’
Pale milango inapokuwa migumu katika eneo ambalo mtu alikuwa analitegemea kumwingizia kipato, kubadilisha fani imekuwa kawaida miongoni mwa wengi, ila kinachozingatiwa ni kama hicho kipya kinampa mhusika fursa ya kutimiza malengo yake ya maisha.
Kujaribu jambo au mbinu mpya ni karba ya binadamu katika kukabiliana na maisha kama ambavyo John Kundwanabake (37) anaamini. Mhitimu huyo wa shahada ya uhandisi wa mifumo ya habari na mtandao ya Chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam, shauku yake katika kilimo biashara imemfanya aiweke kando digrii na kuifuata ndoto yake.
Baada ya kuhitimu masomo yake mwaka 2011, Nkundwanabake alifanya kazi katika tasnia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa miaka miwili tu kupata uzoefu wa alichokisomea akihudumu kama mhandishi wa mashine za kutolea fedha (ATM) kisha akageukia ujasiriamali akifanya kazi kama fundi wa kompyuta na kutoa huduma za Tehama.
Kwa kipindi chote alichokuwa akifanya kazi za taaluma yake, anasema shauku yake ilikuwa kuingia kwenye ujasiriamali wa kuongeza thamani mazao, lakini wakati huo hakujua hasa ni zao lipi alipe kipaumbele, hivyo akalazimika kutafuta maarifa ya kilimo biashara.
“Wakati nikiendelea kufanya ujasiriamali wa Tehama kuna kampuni moja nilikuwa naihudumia ambayo ilikuwa inabangua korosho huko Mtwara. Nikawa nadadisi kuhusu zao hilo na nikajikuta nalifuatilia zaidi na shauku yangu ya kufanya ujasiriamali wa kuongeza thamani kwenye mazao niliona nimepata mwanzo,” anasema Nkundwanabake.
Mwaka 2013 anasema alianza kuuza korosho huku akiendelea na ujasiriamali katika Tehama. Korosho alikuwa anauza kama njia ya kuongeza kipato cha ziada baada ya kuiona fursa, wakati huo aliendelea kuisoma biashara inayohusiana na zao hilo.
Msimu wa mwaka 2014/15 anasema ulikuwa mzuri kwake kibiashara na msimu uliofuata nao ukawa mzuri zaidi, hivyo akaona anapaswa kuweka nguvu zaidi katika eneo hilo. Ili kuongeza nguvu, alianzisha Kikundi cha Wabanguaji Tandahimba (Mivanga Cashewnut) ambacho aling’atuka baadaye.
Anasema kutokana na kuendelea kukua kwa shauku ya biashara ya uongezaji thamani ya mazao, mwaka 2016 alibadili mwelekeo wa kampuni yake ya Tehama (Akros) kuwa ya kilimo na sasa Akros imejikita kwenye korosho, huku Tehama ikibaki kuwa huduma za ziada.
Fursa kwenye korosho
Mpaka miaka ya 1980, historia inaonyesha Tanzania ilikuwa inapata fedha nyingi za kigeni kwa kuuza zaidi zao hilo nje ya nchi, lakini baadaye mambo yakabadilika, ingawa bado kuna fursa ya kurudi katika viwango hivyo kwa kuwa korosho ya Tanzania ndiyo bora kuliko zote duniani.
“Kwenye suala la kuuza nje kwa mfano mdogo wa India, korosho ni kitu ambacho ni lazima kiwepo katika harusi. Kwa mwaka, zaidi ya ndoa milioni 10 hufungwa nchini India. Kama kila harusi watatumia kilo moja ya korosho, mahitaji yatakuwa tani 10 na sisi korosho zetu zinapendwa kuliko za sehemu nyingine,” anasema Nkundwanabake.
Alisema miongoni mwa fursa kubwa zilizopo katika zao la korosho ni ubanguaji, kwa kuwa hivi sasa Tanzania korosho inayobanguliwa ni chini ya asilimia 10 ya kiasi kinachovunwa na mashine za kubangua zipo za ukubwa tofauti na bei yake ikianzia chini hata Sh300,000 mpaka mabilioni.
“Mahitaji ya soko la korosho zilizobanguliwa duniani hatuwezi kuyatosheleza, mfano hapa nchini uwezo wa juu wa viwanda vyetu vyote ni kubangua tani 50,000 na hatujawahi kufikia kiwango hicho. Mwaka jana tumebangua chini ya asilimia tano ya tani 300,000 zilizovunwa,” anasema Nkundwanabake ambaye ni katibu wa Chama cha Wabangua Korosho Tanzania.
Akitolea mfano wa kampuni yake, anasema kwa mwaka anapata oda ya tani 1,400 za korosho zilizobanguliwa, lakini anaweza akakidhi kwa asilimia 30 tu kwa sababu ndizo zilizo ndani ya uwezo wake.
“Ubanguaji ni fursa iliyo wazi kwa watu wengi, ni namna tu unavyojipanga. Sio lazima uanze kwa kubangua kiwango kikubwa, unaweza kuanza kidogo baadaye ukaongeza kikubwa ni kuzingatia ubora. Yeyote anaweza kuchangamkia fursa ya ubanguaji, ila ukikosea kwenye ubora umekwenda na maji,” anasema.
Anasema katika biashara zote zinazohusiana na korosho, yenye hatari kubwa ya kupata hasara ni ubanguaji, lakini zipo nyingine kwa mfano uongezaji thamani wa maganda ya korosho na bidhaa zinazoweza kutengenezwa kwa kutumia mabibo akizitaja kuwa ni juisi na mvinyo.
Serikali na taasisi za fedha
Nkundwanabake anasema taasisi za fedha zinajitahidi kutoa mikopo kwa wajasiriamali waliopo kwenye biashara ya mazao, hususani kwenye kuongeza thamani akisema hata sasa kuna viwanda vikubwa vya kubangua korosho ambayo vipo kwenye upanuzi na vingine vinajengwa kwa mikopo ya ndani.
Anasema Serikali inachopaswa kufanya ili kuinua sekta hiyo ni kuvutia zaidi uwekezaji katika mnyororo mzima wa zao la korosho ili kuiongezea thamani, hali itayofanya korosho yenyewe kuuzwa kwa bei inayovutia wanunuzi wa ndani na nje.
“Ni muhimu kuwa na wawekezaji wengi kwenye mabibo na maganda ya korosho ili mkulima asitegemee manufaa ya korosho peke yake, akipata pesa kwenye hivyo vitu vingine hiyo korosho ataiuza kwa bei rafiki kwa waongeza thamani kama kubangua kwa ajili ya soko la ndani au nje,” anasema Nkundwanabake.
Hatua yoyote ya Serikali kupunguza gharama za uzalishaji korosho kuanzia shambani hadi viwandani, iwapo itachukuliwa, anasema itasaidia kuinua uzalishaji wa zao hilo, uuzaji wake nje ya nchi na kuwanufaisha wakulima wa zao hilo ambalo Tanzania inakusudia kuzalisha wastani usiopungua tani milioni moja ifikapo mwaka 2030.
“Zao la korosho lina uwezo wa kujibu changamoto za ajira kwa vijana wengi, kiwanda kidogo tu ambacho kinaweza kuzalisha kontena moja la korosho zilizobanguliwa unahitaji walau kuwa na watu 100, kwa kuwa korosho inabanguliwa mojamoja hata kama unatumia mashine,” anasema Nkundwanabake.
Kwa kuwa Serikali inalenga kuzalisha tani 700,000 ifikapo mwaka 2025 na kubangua asilimia 60 ya korosho hizo, anasema hakuna budi kutoa vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kwa wawekezaji wa ubanguaji kwa kuwa muda uliobaki ni miaka miwili na sasa uwezo uliopo ni chini ya asilimia 10.