Mabadiliko ya tabianchi yanavyozua migogoro ya binadamu na wanyama
Kasi ya wanyamapori kuvamia makazi imeendelea kuwa tishio katika ustawi wa jamii, huku wadau wakisema hatua hiyo inachagizwa na ongezeko la migogoro kati ya binadamu na wanyama unaotishia mabadiliko ya tabianchi.
Tishio hilo linaakisi wanyamapori 3,340 waliovamia makazi katika wilaya 91 kati ya mwaka 2016 hadi 2019, sawa na watatu waliovamia kila siku kama inavyoelezwa katika Ripoti ya Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Migogoro kati ya Wanyamapori na Binadamu (HWC) wa 2020/24, uliofanyika chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Bila kujali kama walifanya uharibifu wowote katika kijiji husika, wanyamapori hao, wakiwamo tembo, kiboko, mamba, fisi, nyati, simba, chui na nyani walionekana zaidi katika wilaya za Busega, Tunduru, Itilima, Kilombero, Bunda, Bariadi, Manyoni, Serengeti, Rombo na Kilwa.
Mwaka 2016/17 wanyama waliovamia makazi ya watu walikuwa 833, mwaka 2017/18 ni 997 na mwaka 2018/19 wakiwa 1,510, idadi ikiendelea kuongezeka huku matukio ya uharibifu, vifo na majeruhi yakiripotiwa zaidi.
Miongoni mwa matukio hayo ni lile la Mei, 2022 ambalo tumbili zaidi ya 200 walivamia Mtaa wa Nandope FFU, Manispaa ya Mtwara Mikindani na kusababisha uharibifu kwenye bustani za matunda na mbogamboga.
Pia tangu Mei, 2021 hadi sasa, makundi makubwa ya nyani, ngedere na tumbili kutoka katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na hifadhi jirani ya nchini Kenya, yamekuwa yakivamia mashamba na makazi ya watu wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro na kuharibu mazao na kula wanyama wafugwao.
Hata hivyo, John Noronha, Meneja Ufuatiliaji na Tathmini wa Usaid Tuhifadhi Mazingira, anasema msingi wa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori unachagizwa na sababu mbalimbali, ikiwamo ongezeko la idadi ya watu linalochochea uhitaji mkubwa wa ardhi na maliasili.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili, idadi ya watu nchini inaongezeka kwa kasi ya zaidi ya asilimia nne kwa mwaka, huku idadi hiyo ikiongezeka mara nne kati ya mwaka 1967 na 2012, na inakadiriwa kuongezeka hadi kufikia 89.2 milioni ifikapo mwaka 2035.
Sababu nyingine ni ongezeko la matumizi ya binadamu ya njia za maji kwa shughuli za kiuchumi na za nyumbani, mipango ya matumizi ya ardhi na mabadiliko ya tabianchi.
“Pia hakukuwa na mpango madhubuti wa kulinda maeneo yaliyotengwa kujumuisha mfumo mzima wa ikolojia,” anasema Noronha.
“Ardhi ya kijiji ni zaidi ya asilimia 70 ya ardhi yote iliyogawanywa kisheria, na eneo hilo ndipo kuna zaidi ya asilimia 90 ya shoroba zote 61 zilizomo nchini, ni eneo tunalotazama sana katika juhudi za kuondoa migogoro hiyo,” anasema Joseph Olila, Mtalaamu wa Mipango ya Ardhi na Biounuai wa Usaid Tuhifadhi Mazingira.
Kuhusu hoja ya mabadiliko ya tabianchi, Mtaalamu wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Abbas Kitogo mwishoni mwa mwaka jana alinukuliwa akisema kwa sasa Tanzania inachangia asilimia 0.36 ya gesijoto yote inayozalishwa duniani.
Athari na suluhisho
Ripoti hiyo inaakisi watu 1,069 kuuawa na wanyamapori, uharibifu wa ekari 41,404 za mazao na wanyamapori 792 kuuawa huku Serikali ikilipa fidia ya Sh4.6 bilioni kwa mashamba na majeruhi.
Hii ni sawa na wastani wa mwananchi mmoja anafariki dunia kila baada ya saa 52 kwa kujeruhiwa na wanyamapori pamoja na ekari 16 za mazao ya chakula kufanyiwa uharibifu.
Idadi ya vifo vya wanyamapori imeongezeka kwa miaka mitatu mfululizo kutoka 130 mwaka 2017 hadi 149 mwaka 2018 na kufikia 203 mwaka 2019, huku uharibifu wa mazao ya chakula ukiongeza kutoka ekari 5,016 mwaka 2018 hadi ekari 10,547 mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko mara mbili.
Hatua za Serikali
Mwaka jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana aliliambia Bunge kuwa Sh624 bilioni zitatumika kutafuta suluhisho la migongano baina ya binadamu na wanyamapori kupitia utoaji wa elimu na vitendea kazi, kujenga vituo 19 vya kuwadhibiti wanyamapori hao hususani tembo, viboko na mamba.
Hadi Aprili, 2021 wizara ilishapima eneo la hekta 73,528.73 lililogawanywa kwa ajili ya makazi (hekta 10,080.4), kilimo (hekta 13,628.48), malisho (hekta 22,176.06), ujenzi wa taasisi za elimu ya juu na vyuo (hekta 1,329.37), shoroba za wanyamapori (hekta 26,314.42) na hifadhi ya misitu (hekta 6,082.72).
Inachokifanya MCL
Kutokana na changamoto ya vitisho vya mabadiliko ya hali ya hewa, Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), kwa kushirikiana na wadau wa mazingira, itaendesha mdahalo wa kujadili hatua za kuchukua.
Msingi wa mdahalo huo unatokana na Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP-27) uliofanyika Novemba mwaka jana nchini Misri, ukiwakutanisha viongozi wa mataifa mbalimbali duniani.
Meneja Masoko na Uhusiano wa MCL, Vivian Temi alisema mdahalo huo utakaobebwa na kaulimbiu ya “Nini kinafuata kwa Tanzania baada ya mkutano wa COP27” utaangalia matarajio ya sasa na ya baadaye ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa MCL, inayozalisha magazeti ya The Citizen, Mwanaspoti, Mwananchi na Mwananchi Digital, mdahalo huo unawakutanisha pamoja watunga sera, wadau wa mazingira, wataalamu na wananchi kujadili kwa kina fursa na mafanikio yaliyopatikana kupitia mkutano wa COP27.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Seleman Jaffo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mdahalo huo, utakaofanyika Januari 31 jijini Dar es Salaam.