CCM yataja sababu kuwawajibisha watendaji wa Serikali
What you need to know:
- CCM yasema haitaacha kuwahoji watendaji wa serikali wa sekta mbalimbali ili kupata majibu sahihi ya ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili Watanzania.
Morogoro. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amesema katika ziara zake hataacha kuwahoji watendaji wa Serikali kuhusu maendeleo ya miradi mbalimbali ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na wananchi wanapata huduma bora kama ambavyo chama hicho kilivyoahidi katika uchaguzi mwaka 2020, huku akieleza kwamba CCM ndiyo iliyoomba kura kwa wananchi.
Chongolo ametoa kauli hiyo, leo Jumatatu Januari 30, 2023 akizungumza na wananchi na WanaCCM wa Dumila wilayani Kilosa mkoani hapa katika mwendelezo wa ziara yake ya siku tisa ya kukagua uhai wa chama hicho, pamoja na kusikiliza na kutoa suluhisho ya kero zinazowakabili wananchi wa Morogoro.
Katika ziara hiyo, Chongolo amekuwa akisiliza kero za wananchi na kabla ya kutoa uamuzi amekuwa akiwata maofisa na watendaji wa taasisi zinazoguswa kutoa maelezo ya kina kuhusu hatua walizofikia katika utatuzi wa changamoto zinazoelewa na wakazi wa eneo husika.
"Huwa nacheka jana (Jumapili) kuna mtu mmoja ameniambia mbona sasa naita watumishi wa Serikali katika mkutano wangu? Labda niwaulize nani alikuja kuomba kura hapa mwaka 2020 si CCM na mwenyekiti wake ni Rais Samia Suluhu Hassan?
"Sasa Serikali ni ya nani? Tukiiacha tukija kuomba kura tutapewa? si lazima tufuatilie tunahoji na kusimamia ukweli ili tupate matokeo huko mbele. Sasa jamaa wajanja wanataka tusihoji wala kuuliza ili baadaye wasema mliowaona? amehoji Chongolo.
Katika maelezo yake, Chongolo amesema CCM haiko tayari kuona hali hiyo ikijitokeza, watahoji na kufuatilia masuala mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo hadi kieleweke, akisema chama hicho ndicho kilichopewa dhamana ya kuongoza nchi.
"Ukiona unafanya jambo halafu wenzio wanakupigiwa makofi, ujue suala sio nzuri achana nalo. Lakini ukiona unafanya jambo wenzio wanalalamika, liangalie vizuri nyoosha mguu na ongeza bidii ya kulifanya kwa sababu lina maana," amesema Chongolo.
Chongolo aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Longido na Arusha amesema adui hawezi kukufurahi katika jambo la maana, badala yake atakufurahi akiona unaharibikiwa na CCM haipo tayari kuharibikiwa ndio maana inapita kila eneo kutimiza wajibu wa kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi papo hapo.
" Tutawahoji, tutawauliza, tutafuatilia kama hawatekelezi, tutakwenda kujadiliana huko namna nzuri ya mamlaka zinazowahusu kuchukua hatua dhidi yao," amesema Chongolo.
Katika ziara hiyo, Chongolo aliwataka watendaji wa taasisi zinazoguswa na kero za wananchi kukaa sawa na kutekeleza majukumu yao ili kuleta maendeleo kwa wakazi husika na kuwaondolea adha ya kupata huduma bora.
Miongoni mwa changamoto zinazowasilishwa ni pamoja na upatikanaji wa majisafi, umeme, elimu afya na barabara ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa nyakati tofauti kwa wananchi kutaka kupatiwa ufumbuzi.
Kabla ya Chongolo, kueleza hayo Balozi CCM shina la tawi namba 10 la Dumila Juu, Bakari Kimaro amesema eneo hilo lina changamoto za upatikanaji wa umeme, maji katika baadhi yao maeneo wakimtaka katibu mkuu huyo kuyafanyia kazi.
Hata hivyo, watendaji wa sekta za maji na umeme waliopo katika ziara ya Chongolo, kwa nyakati tofauti walimhakikishia katibu mkuu huyo pamoja wananchi wa Dumila kwamba watakwenda kushughulikia na kuzipatia ufumbuzi changmoto zilizoanishwa.
Awali Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Sophia Mjema amesema kazi ya wanaCCM ni kuisimamia Serikali ili kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi na kuleta maendeleo.
" Rais Samia Suluhu Hassan ameleta maendeleo katika sekta za elimu, vituo vya afya, barabara, kilimo na maji. Katibu Mkuu (Chongolo), amekuja kuangalia pia fedha zilizotolewa na Serikali zimetumika vizuri," amesema