LSF yatoa msaada wa kisheria kwa watu 175 kwa siku
What you need to know:
- Wiki ya sheria imehitimishwa jana Januari 29 jijini Dar es Salaam baada kuzinduliwa Januari 22, 2023, ambapo wadau wa mahakama na sekta ya kisheria wamepata nafasi ya kuonyesha kazi zao kwa kutoa huduma kupitia maonyesho hayo.
Dar es Salaam. Katika kuadhimisha wiki ya sheria nchini Shirika la Legal Services Facility (LSF) limetoa msaada wa kisheria watu takribani 175 waluotembelea banda lake lililokuwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini hapa.
Kupitia msaada huo maofisa wa LSF wameshughulikia mashauri yakiwemo migogoro ya ndoa, matunzo ya watoto, mirathi pamoja na migogoro ya ardhi.
Akizungumza jana Januari 29, wakati wa kufunga maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema wamekuwa wakishirikiana na mahakama kukuza upatikanaji wa haki nchini kwa kuwasaidia wananchi kupata haki zao kwa ajili ya maendeleo.
“Wiki ya sheria imekuwa muhimu kwetu kama wadau wa mahakama kwani kupitia wasaidizi wa kisheria tumeweza kutoa huduma bure kwa wananchi waliotembelea banda letu kwa njia ya usulushishi.
"Kupiti wiki hii tumesaidia watu 175 ambapo wanaume ni 73 na wanawake 102,” ameeleza.
Akizungumzia kauli mbiu ya Wiki ya sheria mwaka 2023 isemayo, “Umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi enedelevu endelevu,” Ng’wanakilala amesema, inalenga kuchagiza umuhimu wa wananchi kutafuta haki nje ya mahakama kwa kufanya usulushi.
Naye Msuluhishi kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Usuluhishi, Jaji Dk Zainab Mango amesema kuwa mahakama sasa zinakabiliwa na mashauri mengi yanayoendelea, ambayo pia yanahitaji ushahidi ili kufanya uamuzi wa mwisho.
“Usuluhishi hauchukui muda mrefu, unachukua muda wa siku 30 tu. Hii ni kwa mujibu wa katiba yetu Ibara ya 107A(1)(d), ambayo inasisitiza kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika mgogoro,” amesema.
Dk Mango ameendelea kueleza kuwa usuluhishi unapunguza muda mwingi mahakamani na kumpa muda mteja muda wa kufanya shughuli za kiuchumi.
“Kituo chetu cha usuluhishi kilianza mwaka 2015 na mwaka huu tumetoa taarifa maalum ya utekeleza wa shughuli zetu kwa kipindi cha miaka saba. Kupitia kauli mbiu ya mwaka huu itasaidia kuonesha umuhimu wa usuluhishi kwa wananchi,” amefafanua Dk Mango.
Baadhi ya wananchi waliofika na kunufaika na huduma za usuluhishi katika maadhimisho ya wiki ya sheria wamesema pamoja na changamoto nyingi za kisheria, upatikanaji wa haki umekuwa mgumu kutokana na idadi kubwa ya kesi zinazofikishwa mahakamani.
Joyce Massawe amesema kuwa, amekuwa na mgogoro wa mtoto kati yake na ndugu wa marehemu mume wake, ambao walimnyang’anya bila kufuata utaratibu, lakini maadhimisho ya wiki ya sheria yamesaidia kuweza kupata suluhu.
Naye Filbert Raphael Swabi ameshukuru uwepo wa wiki ya sheria, akisema amepata suluhu kati yake na mkewe Deborah Ernest, baada ya kuwa mgogoro wa ndoa kwa kipindi kirefu bila kupata utatuzi wa kudumu.