Mnyika ataka maadili ya jamii yatafsiriwe kwa Kiswahili
What you need to know:
- Katibu Mkuu wa Chama cha Chadema, John Mnyika amesema mafunzo ya kidini ndiyo msingi wa maadili katika jamii, akisisitiza lugha ya Kiswahili itumike kuyatafsiri.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amesema mafunzo ya kidini ndiyo msingi wa maadili katika jamii, akisisitiza lugha ya Kiswahili itumike kuyatafsiri.
Mnyika ameyasema hayo leo, Januari 30, 2023 jijini Dar es Salaam, katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha IBN KATHIR chenye tafsiri ya kitabu kitukufu cha Quran, uliofanywa na Taasisi ya IBN Hazm.
Kulingana na Mnyika, hatua ya taasisi hiyo kukitafsiri kwa Kiswahili Kitabu hicho itachagiza mafunzo kuwafikia wengi, lakini itakuza lugha hiyo.
"Kitendo cha kutafsiri kwenda lugha ya Kiswahili itachangia kukua kwa lugha hiyo, hata katika nchi zisizozungumza Kiswahili," amesema.
Ameeleza umuhimu wa mafunzo ya dini katika jamii, akisisitiza umuhimu wa watu wa imani zote kujenga utaratibu wa kusoma vitabu mbalimbali.
"Kwa kuwa Kitabu hiki kimetafsiriwa kwa Kiswahili, kitawezesha watu wa imani zote kusoma," ameeleza.
Naibu Mufti wa Zanzibar, Mahmoud Wadi ambaye amemuwakilisha Mufti wa Zanzibar, amesema kutokana na lugha iliyotumika watu wengi watajifunza na kuelewa maudhui yaliyomo kwenye Kitabu hicho.
"Kwakweli leo tumeingia kwenye historia ya kielimu kwenye nchi yetu hata kwa nchi nyingine zinazozungumza lugha ya Kiswahili, kwa ile faida kubwa tutakayoipata wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili kwa kusoma kitabu hiki," amesema.
Sheikh Ponda Issa Ponda, ni miongoni mwa wadau waliohudhuria uzinduzi huo, amesema kitafungua uelewa wa wengi.
"Vitabu vingi vya mafundisho ya kiimani vimewekwa kwa lugha ya kigeni kama Kiingereza na Kiarabu kwa hiyo, kupitia tafsiri hii watu wataweza kufaidika sana," amesema.
Said Bawazir ni mmoja wa waliotafsiri Kitabu hicho, amesema wasomaji watapata utambuzi na ufahamu mkubwa kwa mambo ya Mwenyezi Mungu, hivyo wanapaswa kusoma.
"Watu wafahamu maneno ya Mwenyezi Mungu na anataka wanadamu wafanye nini na hili litasaidia hata Amani," ameeleza.