Taasisi tatu zinazoongoza viashiria uvunjaji maadili, Polisi wamo
What you need to know:
- Serikali imetaja Taasisi za Polisi, Mahakama na Muhimbili kwamba zinaongoza kwa viashiria vya uvunjifu wa maadili nchini hivyo akaomba viongozi wakutane na kujadili kwa nini taasisi nyeti kama hizo zinatajwa.
Dodoma. Serikali imetaja taasisi za Polisi, Mahakama na Muhimbili kwamba zinaongoza kwa viashiria vya uvunjifu wa maadili nchini hivyo akaomba viongozi wakutane na kujadili kwa nini taasisi nyeti kama hizo zinatajwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Januari 30, 2023 wakati akizungumza na watumishi wa wizara yake ambapo amesema kiwango cha uzingatiaji wa maadili katika utumishi wa umma kwa mwaka huu kimeongezeka hadi asilimia 75.9 ikilinganishwa na mwaka 2014 ilipokuwa asilimia 66.1.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao kazi cha usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kilichojadili matokeo ya utafiti wa uzingatiaji wa maadili katika utumishi wa umma mwaka 2022,Waziri Mhagama amesisitiza wajumbe wa kikao hicho kuhakikisha wanabaini kwa nini taasisi hizo zinaendelea kuongoza na nini kifanyike ili kuondokana na changamoto hiyo.
"Kufanya utafiti ni kazi moja na kutoa matokeo ya utafiti ni jambo lingine, hivyo nendeni mkahakikisheni unapokea taarifa, mkayabaini yaliyoko kwenye tafiti hizo na kuyafanyia kazi," amesema Mhagama.
Waziri Mhagama amesema ongezeko la matokeo hayo linatokana na jitihada za kuimarisha uzingatiaji wa maadili ambapo utafiti unaonyesha juhudi za serikali za kuchukua hatua katika kuweka misingi imara ya usimamizi wa maadili, kuweka mazingira wezeshi na kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa umma.
Amemwagiza Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, kufanya kikao kazi cha pamoja na wadau kwa ajili ya kufanya mjadala wa kina kuhusu matokeo ya utafiti ili wapange mikakati ya ufuatiliaji wa uzingatiaji wa maadili katika sekta zilizotajwa.
Katika hatua nyingine ameagiza waajiri kuhakikisha wanatenga bajeti ya mafunzo ya maadili na kuendesha mafunzo kwa watumishi wa umma walio kazini na wanaoajiriwa kwa sasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi na Utawala Bora, Cosmas Ngangaji amesema usimamizi kwa kutumia Sera na usimamizi wa rasilimali watu katika Utumishi wa umma utawafikisha malengo na matarajio ya Serikali na ametaka mpango huo kushuka hadi ngazi ya vitongoji na mitaa.