Wadau waungana kupinga sheria kandamizi za habari
Dar es Salaam. Wadau wa habari nchini Tanzania wameendelea kusisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kuwa huru ili kuweka mizania sawa ya uhuru katika upatikanaji na upashanaji taarifa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Hii itatokana na Serikali kuridhia mabadiliko na maboresho ya kanuni na sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambayo kwa sasa maoni yanakusanywa ili kuirejesha bungeni.
Katika kuliona hilo, Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (Misa-Tanzania) inawakutanisha wadau hususan wanahabari kueleza sheria hizo ikiwemo ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA).
Akitoa mada, mwandishi mwandamizi, Jesse Kwayu alisema sheria hizo na zingine zinazosimamia tasnia ya habari zinapaswa kufanyiwa mabadiliko kwani zinawabana na kuwafanya wanahabari kufanya shughuli zao kwa hofu.
Kwayu alisema kuna baadhi ya vifungu vinatoa adhabu kali kwa chombo cha habari na mwandishi mwenyewe, hivyo kuwafanya waandishi kuwa waoga na kutoisaidia vyema Serikali.
“Taaluma inatuongoza kulinda vyanzo vya habari, lakini sheria hii ya EPOCA kuna adhabu ya faini au kifungo kisichopungua mwaka mmoja au vyote kwa pamoja pale inapotokea umekataa kutaja vyanzo,” alisema Kwayu ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Brain Incorperated
Kwayu alisema, “ukishakuwa na sheria mbaya huwezi jua saa ngapi itakukamata. Tusilale tusome, tupige kelele kuhusu sheria zinazokandamiza, hizi sheria bado hazijarekebishwa, tupo kwenye mchakato ambaop ni lazima tushiriki kwa kuwa inatuhusu.”
Katika mahojiano na Mwananchi kuhusu sheria hizo, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema wanasiasa wanapaswa kusimamia marekebisho hayo kikamilifu ili demokrasia na uhuru wa habari vishamiri.
Zitto alisema wakati sheria ya huduma ya vyombo vya habari inapitishwa alikuwepo bungeni na waliipinga kwa kuwa walijua inaminya uhuru wa habari na demokrasia na inatoa fursa zaidi ya utashi wa mtu kuamua mambo
“Nchi iliendeshwa gizani waati huo ndiyo maana haikuwa ajabu kwa sheria kandamizi kupitisha lakini sasa naona mambo ni tofauti, hali inakwenda vizuri lakini tunapaswa kutengeneza sheria bora zinazozuia utashi wa watu kuamua mambo,” alisema
Zitto alisema jambo la kutia moyo hivi sasa ni kuona Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewashirikisha wadau katika mchakato wa marekebisho ya sheria, hivyo kitakachopelekwa bungeni kinaweza kutatu mkwamo uliokuwapo
Naye Mwenyekiti Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alisema wanaamini muswada uko kwenye hatua nzuri kwa kuwa Waziri Nape alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali anakamilisha taratibu zinazotakiwa kabla ya kuingia bungeni.
“Tunajua kila kitu kina taratibu zake, katika awamu hii tumeshirikishwa na tumetoa maoni yetu, tunaamini utafikishwa katika Bunge linaloanza vikao vyake leo na tutapata sheria bora itakayotukwamua hapa tulipo” alisema
Mwandishi wa habari, Shomari Jemedari alisema anaamini wabunge watafanya marekebisho kwa kuzingatia masilahi ya umma ili kuchochea uhuru wa habari na ukuaji wake.
Alisema anaamini sheria ilipotungwa kulikuwa na dhamira ya kudhibiti sauti za watu hasa wakosoaji lakini hivi sasa mazingira ni tofauti hivyo sheria kandamizi zinapaswa kurekebishwa
Kwa upande wake, mwandishi wa habari wa kujitegemea, Susan John alisema ana wasiwasi muswada huo unaweza kupelekwa kwa hati ya dharura hivyo wadau watashindwa kuuboresha zaidi.
“Nina uzoefu na hii miswada, mpaka wiki iliyopita nilisikia hata kwenye kamati ya Bunge inayohusika nayo haukuwa umefika, hivyo nachelea kusema ukitoka kwa AG utapelekwa kwa hati ya dharura na hapo ndipo tutakapoumia,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Misa-Tanzania, Salome Kitomari alisema Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 inakwamisha uwekezaji katika sekta ya habari hasa kwa wawekezaji kutoka nje.
Alisema Sheria ya Huduma za Habari inakwamisha uwekezaji kwa sababu watu wenye mitaji kutoka nje ya nchi hawataweza kuja kuwekeza kwa sababu sheria inataka mwekezaji wa ndani kuwa na umiliki wa asilimia 51 wakati wa nje akitakiwa kuwa na asilimia 49 pekee.
“Sisi kama wadau tumeona kwamba kuna kikwazo katika kuruhusu ustawi wa vyombo vya habari. Tunajiuliza, mtu kutoja nje anaweza kuja kuwekeza fedha yake wakati yeye ni mdogo katika ule uwekezaji?”
“Mtu anataka akiwekeza awe na uhakika kwa kile anachowekeza, kwa hiyo tunaona ni vizuri serikali ikalianglia hilo katika jicho la ustawi. Sekta ya habari imeajiri watu wengi sana lakini pia inachangia ukuaji a uchumi wa nchi hii,” alisema.
Mwenyekiti huyo aliongeza kukiwa na uwekezaji katika sekta ya habari kama ilivyo kwenye sekta nyingine, maana yake vyombo vya habari vitastawi na kuisaidia nchi kupitia mapato ya kodi na ajira kwa wananchi.
“Muswada huu ukifika bungeni, wabunge waungalie vizuri katika jicho chanya kwa kuzingatia manufaa makubwa ambayo yatapatikana,” alisema Kitomari na kusisitiza sheria hiyo ya sasa imekuwa kizuizi.
Mwanahabari huyo alibainisha jambo jingine kwamba leseni za wanahabari zisiwe za mwaka mmoja mmoja, bali zitolewe angalau kila baada ya miaka mitano ili hilo lisitumike kama fimbo ya kuwaadhibu wanahabari na pia kuwapa uhakika wa kazi yao.