Zitto Kabwe atoa mapendekezo muswada wa bima ya afya kwa wote
What you need to know:
- Serikali itawasilisha bungeni kwa mara ya pili muswada huo baada ya kuondolewa mwaka jana kutokana na kile kilichoelezwa, ni kukosekana kwa chanzo halisi cha mapato ya kuwezesha kutoa huduma hizo kwa wote.
Dar es Salam. Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameshauri kufungamanishwa mifuko ya hifadhi ya jamii na bima ya afya ili iwe kama mafao ndani ya mifuko hiyo.
Zitto ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza kesho Januari 31, 2023 jijini Dodoma ambapo miongoni mwa miswada itakayowasilishwa ni pamoja na ule wa bima ya afya kwa wote.
Serikali itawasilisha bungeni muswada huo kwa mara ya pili baada ya kuondolewa mwaka 2022 kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kukosekana kwa chanzo halisi cha mapato ya kuwezesha kutoa huduma hizo kwa wote.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Digital leo Jumatatu Januari 30, 2023 ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Zitto ametoa mapendekezo ambayo yatasaidia kukuza mfuko wa bima ya afya ili usaidie Watanzania wote.
Asema katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), kuna fao la matibabu ambalo halitumiki tangu mwaka 2019 kutokana na Serikali kuliondoa huku wanufaika wa fao hilo wakibaki waliojiunga na mfuko huo kuanzia mwaka 2018 kurudi nyuma.
Zitto amesema fao la matibabu lipo kisheria na bodi ya NSSF haina mamlaka ya kulizuia, hivyo haina budi kuliachia litumike.
“Watu wanaochangia fao la matibabu na NSSF wako milioni moja na nusu sawa asilimia 20 ya makusanyo yote ambayo mfuko huo unakusanya, hivyo yachukue na kuyapeleka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
“Kwa hatua hiyo pekee yake ndani ya mwaka mmoja kiwango cha fedha ambacho NHIF itakipata Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na NSSF kwa idadi ya walioko sasa ni zaidi ya Sh530 milioni ambayo ni asilimia 20 ya michango yote na hili ni jambo ambalo limefanyiwa mahesabu na watu wa bima,” ameeleza Zitto.
Katika hatua nyingine, Zitto amesema kwa watu ambao wamejiajiri kwa shughuli mbalimbali wakiwamo wamachinga na wakulima wanaweza kuingiza kipato cha juu kuzidi hata walioajiriwa lakini hakuna kivutio chochote cha kuwafanya wajiunge na mifuko ya hifadhi ya jamii.
Zitto ameshauri Serikali ione namna ya kuwashawishi watu wa aina hiyo kujiunga katika mifuko hiyo.
Vilevile, Zitto amegusia suala la Watanzania wa kipato cha chini ambao wengine wapo chini ya Mpango wa Kusaidia Kaya Maskini (Tasaf), akishauri walipiwe mafao katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
“Badala ya kuendelea kuwapa tokeni kwa mwezi ni bora walipiwe asilimia 100 kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii ambayo siyo tu watapata matibabu lakini pia watapata fao la mikopo ambalo litawatoa kwenye hali duni na kuwaweka kwenye hali nzuri,” amesema Zitto akitoa mapendekezo ya chama chake.
Zitto amesena endapo Serikali ingeyafuata mapendekezo hayo, basi kiwango cha fedha ambacho NHIF ingekikusanya kwa mwaka wa kwanza kingetosha kumfanya kila Mtanzania awe na bima ya afya.