Mbrazili mwingine atimka Singida Big Stars
NYOTA wa Singida Big Stars, Dario Frederico amesema kwa sasa amerejea Brazil kwa ajili ya mambo ya kifamilia huku akiwatoa hofu mashabiki zake atarejea muda sio mrefu kuendelea na majukumu kama kawaida.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka Brazil, Dario alikiri kuondoka nchini kwa ruhusa maalumu ya viongozi na kueleza hakuna mgogoro baina yake na waajiri wake kama inavyoelezwa baada ya kuondoka kwake.
“Sina mgogoro wowote na viongozi wangu, hivyo nipende kuwahakikishia mashabiki na wachezaji wenzangu nipo kwa ajili ya kuipigania timu na muda siyo mrefu tutajumuika tena pamoja kuendeleza harakati zetu,” alisema.
Kwa upande wa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Singida, Muhibu Kanu alisema mchezaji huyo ameomba ruhusa kwa ajili ya kutatua matatizo yake ya kifamilia na suala la kuondoka kwenye timu yao sio kweli.
Dario anakuwa mchezaji wa tatu kuondoka Singida Big Stars kwa ajili ya masuala ya kifamilia baada ya Mbrazili mwenzake, Peterson Cruz na Muargentina, Miguel Escobar ingawaje wawili hao hawakuweza kurudi tena nchini kwani walipata timu nyingine.